Zikiwa zimebaki wiki mbili kuanza vikao vyake, baadhi ya wanasheria wamehoji uhalali wa Bunge hilo kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba bila ya kuwapo kwa wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Wamesema msimamo wa Ukawa kukataa kurejea katika
vikao vya Bunge hilo na kushikilia msimamo wa kutaka ijadiliwe Rasimu ya
Katiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, utafanya akidi ya wajumbe kwa
ajili ya kupitisha uamuzi katika Bunge hilo kutotimia.
Wanasheria hao waliohojiwa jana kuhusu msimamo wa
Ukawa kususia Bunge na hatima ya Katiba Mpya wamesema hakuna uwezekano
wa kisheria kuipitisha wala kufanya mabadiliko ya vifungu ili kupata
uhalali wa kufanya hivyo.
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili Julai 8
mwaka huu, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta alisema
iwapo Ukawa watarudi bungeni lakini wakasusa tena kadri mjadala
utakavyoendelea, Bunge litaangalia upya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
ambayo inataka theluthi mbili kufanya uamuzi.
Hata hivyo, wanasheria hao walisema kwamba bila
kuwapo maridhiano, Bunge hilo haliwezi kufikia tamati na si rahisi
kupata akidi ambayo si tu inatakiwa na Kanuni za Bunge na Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, bali pia Katiba ya sasa.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Kifungu cha 26(2)
kinaeleza: “Ili Katiba inayopendekezwa iweze kupitishwa katika Bunge
Maalumu, itahitaji kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya idadi ya
wajumbe wote wa Bunge Maalumu kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya
idadi ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu kutoka Tanzania Zanzibar.”
Wakili na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Jesse James alisema iwapo hakutakuwa na maridhiano hakuna
chochote kinachoweza kufanyika au kupitishwa zaidi ya kuahirisha Bunge
hilo hadi pale watakapokubaliana.
“Hakuna kifungu cha sheria kinachosema Rais
anaweza kulivunja Bunge hilo, bali linaweza kuahirishwa. Nami
ningeshauri liahirishwe hadi hapo maridhiano yatakapopatikana,” alisema
James.
Kuhusu kubadilishwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba ili kubadili akidi ya wajumbe wa pande zote mbili, James alisema
hilo litasababisha vurugu zaidi.
Alisema hilo linaweza kufanyika kwa kuitishwa kwa
Bunge la Muungano, lakini kwa maoni yake itakuwa ni uhuni kwa kuwa
haiwezekani kubadilisha kanuni wakati mchezo umeshaanza.
“Wakifanya hivyo itakuwa ni vurugu tupu, watakuwa
wanapitisha kwa matakwa yao kitu ambacho kitaleta shida wakati
itakapowasilishwa kwa wananchi kwa ajili ya upigaji kura,” alisema James
na kuongeza:
“Wakati wa upigaji kura italeta shida kwani hawa
ambao hawakubali watapiga kampeni kuwaeleza wananchi wasiikubali kwa
kuwa si matakwa yao na hapo itakuwa vurugu zaidi.”