Matukio
ya kukata viungo vya walemavu wa ngozi (albino), yameendelea mkoani hapa,
ambapo juzi mlemavu wa pili katika muda usiozidi wiki mbili, amekatwa kiwiko
cha mkono wake na wahusika kutoweka nacho kusikojulikana.
Suzana
Mungi (35) ambaye ni mlemavu wa ngozi na mkazi wa Kijiji cha Buhelele kata
ya Nsimbo wilayani Igunga, amekatwa kiwiko cha mkono wake na wahusika kutoweka nacho
kusikojulikana.
Katika
tukio hilo lililofanyika juzi, mume wa Suzana, Mapambo Mashili ameuawa kikatili kwa
kupigwa na kitu chenye ncha kali kifuani na kichwani wakati akijaribu kumnusuru
mkewe asikatwe mkono wake.
Hivi
karibuni mtoto Upendo Sengerema (15), mkazi wa Kijiji cha Usinge, Kata ya
Uganza Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, alikatwa mkono na wahalifu ambao
walikimbia nao. Mpaka sasa Upendo amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Urambo
mkoani hapa.
Akizungumzia
tukio hilo jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Mkuu wa
Mkoa wa Tabora, Fatma Mwassa (pichani), alisema
kitendo hicho ni cha kinyama, ambacho hakiwezi kuvumiliwa na mtu yeyote.
Alisema
watu wote watakaobainika kufanya unyama huo, watachukuliwa hatua kali za
kisheria ili kukomesha vitendo hivyo visivyokuwa vya kistaarabu.
Aidha,
aliwataka wakuu wa wilaya zote mkoani hapa, kutambua maeneo yote ambayo
wanaishi walemavu wa ngozi na kuwa karibu nao kwa ajili ya kuimarisha ulinzi
wao kila siku katika maeneo wanayoishi.
Mkuu
wa huyo wa Mkoa, ametangaza dau la Sh 500,000 kwa mwananchi yeyote atakayetoa taarifa za kupatikana kwa
wahalifu wanaojihusisha na matukio hayo.
Pia,
Mwassa aliliagiza Jeshi la Polisi mkoani Tabora, kuhakikisha waliofanya matukio
hayo, wanakamatwa na kutiwa mbaroni na
kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.
Kamanda
wa Polisi mkoani Tabora, Suzana Kaganda,
aliwataka wakazi wa Mkoa wa Tabora, kuachana na imani za kishirikina na
kueleza kuwa atahakikisha wahusika wanakamatwa.